Mfanyabiashara wa soko la Saateni Khamis Ali
Mohd akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad kuhusiana na hali ya kudorora kwa biashara katika soko hilo, wakati
Maalim Seif alipotembelea eneo hilo jana.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad akiulizia bei ya viatu, wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo
la biashara la Saateni mjini Zanzibar.maaarufu kwa jina la jua kali.
Mfanyabiashara ya mitumba katika soko la
Saateni akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad alipotembelea eneo hilo jana.

Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia biashara ya mitumba, wakati
alipofanya ziara ya kutembelea eneo la biashara la Saateni mjini Zanzibar.(Picha
na OMKR)
Makamu wa Kwanza wa
Rais Maalim Seif Atembelea Wafanyabiashara Jua Kali.
Na Hassan Hamad
(OMKR).Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad ameelezea umuhimu wa kutafutwa muwekezaji kwa ajili ya kulijenga na
kuliendeleza soko la saateni, ili kuweka mazingira bora ya kibiashara katika
soko hilo.
Amesema mazingira yaliyopo sasa hayaridhishi kutokana na
kutokuwa na miundombinu imara, hali inayowafanya baadhi ya wafanyabiashara
kufikia uamuzi wa kulihama soko hilo na kuelekea darajani, eneo ambalo
haliruhusiwi kwa wafanyabiashara wadogowadogo.
Maalim Seif ametoa kauli
hiyo leo alipofanya ziara ya kutembelea soko la Saateni kuangalia hali ya
biashara inavyokwenda hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
Amesema iwapo soko hilo litaimarishwa na kuwekewa miundombinu ya
kisasa, litaweza kuwavutia wafanyabiashara wengi na kupunguza tatizo la ajira
kwa vijana ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakikabiliwa na tatizo
hilo.
“Dawa ya kuwadhibiti wafanyabiashara wadogo wadogo walioko darajani
ni kulijenga eneo la Saateni na kuwekea miundombinu ya kisasa, wala haina haja
ya kutumia nguvu, watakuja wenyewe Saateni”, alifahamisha Maalim
Seif.
Aidha ameuagiza uongozi wa baraza la manispaa Zanzibar kuharakisha
ujenzi wa vyoo katika eneo hilo, ili kuwaondoshea usumbufu wafanyabiashara na
wananchi wanaofika katika eneo hilo.
“Naomba kwa sasa kipaumbele kiwe ni
ujenzi wa vyoo kwani wananchi wanaofika katika eneo hili na wengi na bila shaka
watakuwa wanasumbuka”, aliagiza.
Sambamba na hilo, Makamu wa Kwanza wa
Rais amesema soko la Saateni linaweza kuimarika zaidi iwapo kituo cha daladala
cha darajani kitahamishiwa katika eneo hilo.
Kwa upande wao
wafanyabiashara wa Saateni wamesema hali ya biashara katika eneo hilo sio nzuri,
hali inayotokana na wananchi wengi kufikia eneo la darajani na kumalizia
shughuli zao za kibiashara katika soko hilo.
Wamesema ni vigumu kwa sasa
wananchi kwenda katika soko la saateni kutokana na usumbufu uliopo wa daladala,
na kuomba kituo cha daladala kihamishiwe eneo la Saateni ili kuwawezesha
wananchi kufika moja kwa moja katika soko hilo.
“Hatuwezi kuwa na masoko
mawili katika nchi hii ndogo, tunaomba kituo cha daladala kihamishiwe Saateni
kama tulivyoahidiwa, na serikali kutowaonea muhali wafanyabiashara wenzetu
wadogowadogo walioko darajani, wawahamishe wawalete huku tuungane la si hivyo na
sisi tutarejea darajani”, alitanabahisha mfanyabiashara mmoja wa soko hilo
aliyejitambulisha kwa jina la Makame Mussa.
Mfanyabiashara mwengine wa
soko hilo nd. Khamis Ali Mohd amesema biashara zao zimekuwa zikiyumba kutoka na
wafanyabiashara wa Darajani kuendelea kuweko huko, na eneo la Saateni
kusahauliwa kabisa kibiashara.
“Mimi ni mjenzi ambaye nililazimika
kujenga milango kadhaa kutokana na ahadi tuliyopewa kuwa wafanyabisahara wa
darajani wote watakauja huku, hivyo nilijenga kutokana na makubalianao yetu na
manispaa kuwa asilimia 50 ya milango niwakodishe wafanyabiashara wanaotoka
darajani, lakini hadi leo hakuna aliyekuja”, alilalamika Khamis huku akionyesha
milango yake kadhaa iliyofungwa kwa muda mrefu bila ya kufanyiwa biashara
yoyote.
Amesema awali alipanga kukodisha milango hiyo kwa shilingi 70
elfu kila mmoja lakini ameshindwa kupata mteja hata wa shilingi 40 elfu,
kutokana na mwenendo mbaya wa biashara unaosababishwa na kuweko kwa
wafanyabiashara na kituo cha daladala katika eneo la darajani.
Ameiomba
serikali kufuatilia kwa karibu uimarishwaji wa soko la Saateni, ili kulifanya
kuwa soko kubwa la kisasa litakalovutia wafanyabiashara wakubwa na wadogo, na
hatimaye kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Kwa upande mwengine
wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuweka matuta
katika eneo hilo ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza.
Nae Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mwinyihaji Makame
amesema serikali inaweka utaratibu wa kuweza kuwahamisha wafanyabiashara wadogo
wadogo wa darajani ili waweze kuungana na wenzao walioko Saateni.
“Ukweli
soko la darajani limevamiwa, hata ukienda katika eneo linalouzwa bidhaa za
vyakula, lakini imebidi tufumbie macho kidogo kwa kipindi hiki, ili kupunguza
usumbufu kwa wananchi wanaotafuta huduma mbalimbali ikizingatiwa kuwa ni mwezi
mtukufu wa Ramadhani”, Alisema Dkt. Mwinyihaji Makame.
Waziri wa
Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, kwa upande wake aliahidi
kuimarisha mazingira ya kibiashara katika soko hilo, na kusisitiza haja ya eneo
hilo kuwa ndio kituo kikuu cha daladala “bus stand”.
Hassan Hamad
(OMKR).