Pages

Thursday, August 29, 2013

UTANDAZAJI MABOMBA YA GESI MTWARA-DAR

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiwa na Balozi wa China nchini, Lu Youqing walipokuwa wakikagua mitambo ya kisasa ya kuunganisha mabomba ya kusafirishia gesi, katika karakana namba tano  ya Kampuni ya kichina ya CPTDC ya Ikwiriri, wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani .Profesa Muhongo alifanya ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa maandalizi ya utandazaji wa mabomba hayo ya gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa  Kampuni ya kichina ya CPTDC iliyopewa tenda ya kutandaza mabomba ya gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, alipokuwa katika ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa maandalizi ya utandazaji wa mabomba hayo ya gesi, juzi eneo la Somanga Fungu, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.
 Sehemu ya mabomba ya gesi yakiwa eneo la kuhifadhia la Nyamwage, Rufiji
 Profesa Muhongo akiangalia kipenyo cha bomba ambacho ni mita moja
 Profesa Muhongo akioneshwa sehemu ya bomba itakayounganishwa na bomba lingine
 Watalaamu wa ubora wa ufungaji mabomba ya gesi kutoka Afrika Kusini wakimueleza Waziri Muhongo kuhusu umakini wakati wa kuunganisha mabomba hayo
 Profesa Muhongo akiwa eneo la kuhifadhia mabaomba, Nyamwage, wilayani Rufiji. Mabomba hayo yalianza kuunganishwa jana.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia), akizungumza na baadhi ya vibarua  wa kitanzania wanaofanya kazi katika kampuni hiyo ya kichina katika kambi ya kuhifadhia mabomba ya Nyamwage, wilayani Rufiji, Pwani.
 Waziri Muhongo akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kamapuni hiyo ya kichina.
  Kamanda Richard Mwaikenda naye akiwa katika ziara hiyo eneo la Nyamwage, Rufiji.
 Kambi ya wafanyakazi wa kamapouni ya kichina eneo la Mkuranga, Dar es Salaam
 Waandishi wa habari walioambatana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (amezibwa), wakiangalia nyaya za mkongo zitakazotandazwa sambamba na mabomba ya gesi kwa ajili ya usalama, zilizokuwa kwenye lori katika ghala la kampuni hiyo ya kichina wilayani Mkuranga, Pwani
Baadhi ya mitambo ikiwa imefungwa wilayani Mkuranga, Pwani, kwa ajili ya kuongezea unene wa mabomba maalumu ya gesi yatakayotandazwa baharini.

Serikali yaridhishwa na kasi ya ujenzi wa bomba la gesi

Serikali imeridhishwa na kasi ya kazi inayofanywa ya mradi wa kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Hayo yalibainika wakati Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Balozi wa China nchini, Lu-Youging walipofanya ziara ya pamoja kukagua ujenzi wa bomba hilo. Katika ziara hiyo walitembelea kambi tano za mradi za Somangafungu, Nyamwage, Ikwiriri, Mkuranga na Kongowe katika Mto Mzinga.
Waziri Muhongo alisema ameridhishwa na kasi ya kazi inayofanywa ya mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam huku akiwataka watanzania kuwa na imani na kazi hiyo.
Alisema awali zoezi hilo lilitakiwa kukamilika mwezi Januari, 2015, lakini huenda likawahi kumalizika kutokana na kuwepo kwa vifaa vya kisasa na imara kutoka Kampuni ya China Petroleum Pipeline (CPP) watakao fanya kazi ya kulitandaza.
Alisema mabomba hayo ni imara na yanaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 70 iwapo yatatunzwa vizuri na kwamba serikali itahakikisha inayafuatilia vizuri na kuhakikisha hayachafuki
Waziri Muhongo alisema kazi ya kuunganisha vipande vya bomba inaanza rasmi tarehe 26 Agosti na wakati huo uchimbaji ukiendelea kwa ajili ya kuweka mabomba hayo ambayo yatakuwa tayari yameunganishwa.
“Uunganishwaji unafanywa na mitambo ya kisasa kabisa na hapo bomba linapochimbiwa ndio hapohapo uunganishaji unafanyika na bomba zitakazolazwa baharini zitaunganishwa hukohuko” alisema.
Alisema kwa bomba zitakazoenda baharini uzito wake ni mkubwa zaidi ikilinganishwa na bomba zitazotumika nchi kavu kwakuwa zitakazolazwa baharini zitawekewa zege maalumu.
“Bomba zitakazoenda baharini zitakuwa na uzito wa zaidi ya tani 10 baada ya kuwekewa zege ambapo kwa sasa zina uzito wa tani tatu” alisema.
Alisema kazi ya kutandaza mabomba baharini itaanza Septemba 16, mwaka huu kwa kuwa kazi hiyo inahitaji umakini mkubwa.
Profesa muhongo alisema pindi bomba hilo litapokamilika uzalishaji wa umeme utaongezeka kutoka megawati 1500 zilizopo hadi kufikia megawati 3000 mwaka 2015 na kuanza kuuza umeme utakaokuwa wa ziada kwa nchi jirani.
Kuhusu suala la ajira, Waziri alisema mradi huo tayari umezalisha ajira. Alisema magari ya watanzania yapatayo 45 yamepewa kazi ya kusafirisha mabomba huku watanzania wengine wakiajiriwa katika kazi zinazoendelea.
Balozi wa China nchini, Lu Youging alisema mradi huo ni wa kipekee na una umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wa Tanzania kwani kupitia mradi huo, Tanzania itaweza kuwa na viwanda vingi na kupelekea kuongezeka kwa ajira nchini.

Aliongeza kuwa mradi huo utasaidia katika utunzaji wa mazingira kwakuwa badala ya kuendelea kukata miti kwa ajili ya mkaa na kuni, watanzania watatumia gesi asilia kwa matumizi ya kupikia.

No comments:

Post a Comment