Pages

Monday, January 21, 2013

RAIS wa ZFA AMAN MAKUNGU ATAKA KUJIUZULU!!


  
ZANZIBAR_STONE_TOWNRais wa Chama cha Mpira wa Miguu Visiwani Zanzibar (ZFA), Aman Ibrahim Makungu, ameandika barua ya kutaka kujiuzulu nafasi yake kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuchoshwa na vitendo vya baadhi ya Viongozi wa juu wa Chama hicho cha kukataa mabadiliko chanya.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika chanzo cha kuaminika, ni kuwa barua ya Rais Makungu iliyoandikwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji Salum, ambayo imesainiwa na yeye mwenyewe imesema kuwa amechoshwa na tabia ya baadhi ya Viongozi wa juu wa Chama hicho cha kukataa kumpa ushirikiano, huku lawama nyingi akizielekeza kwa Katibu wake Mkuu na Makamu wa Rais kisiwani Pemba akiwataja kuwa ndio chanzo cha kukosekana ushirikiano katika Chama hicho.
Hata hivyo barua hiyo inatarajiwa kukabidhiwa rasmi kesho kutwa mara baada ya kumalizika kwa ziara rasmi ya ZFA katika Wilaya nne za Pemba, ziara ambayo inamalizika kesho katika Wilaya ya Chake Chake.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara rasmi ya Viongozi wa ngazi za juu wa ZFA wakiongozwa na Rais mwenyewe Aman Makungu, kwenda kisiwani Pemba kwa lengo la kuzungumza na Viongozi wa soka katika wilaya zote za Pemba na ziara hiyo kudaiwa kususiwa na Viongozi wa juu wa ZFA kisiwani Pemba akiwemo Makamu wa Rais kisiwani Pemba pamoja na Msaidizi Katibu wa ZFA kisiwani Pemba.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na hali ya kutokuelewana kwa Viongozi wa juu wa ZFA kati ya Unguja na Pemba huku kila upande ukiwa na sababu zake, wakati uongozi wa ZFA kisiwani Unguja ukilezea tabia ya Viongozi wa Kisiwani Pemba kufanya mambo kienyeji, Uongozi wa ZFA kisiwani Pemba umekuwa ukilalamika juu ya maamuzi makubwa yanayofanywa na Chama hicho bila ya kuwashirikisha huku wakitolea mfano wa suala la kufungiwa kwa Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes'.

No comments:

Post a Comment