Pages

Friday, April 26, 2013

Rais Kikwete aongoza maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete,akisalimiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk.Ali Mohamed Shein,alipowasili katika Uwanja wa Uhuru wa Jijini Dar es Salaam, katika Kilele cha Maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano wa Tanzania zilizofanyika leo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, leo aliwaongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Sherehe hizo zilifanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa nchini, mawaziri wa Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar, viongozi wa ngazi zote na watendaji wakuu pamoja na wananchi mbalimbali.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Peter Pinda.
Wengine ni Marais wastaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Mawaziri Wakuu wastaafu Fredrick, Sumaye, Edward Lowasa na John Malecela, Spika wa Bunge Anne Makinda na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na viongozi wengine.
Pamoja na mvua ya wastani iliyokuwa ikinyesha mapema asubuhi, wananchi mbalimbali walijitokeza kwa wingi uwanjani hapo kusherehekea Muungano huo wa kihistoria ulioziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, mwaka 1964.

No comments:

Post a Comment