Pages

Thursday, May 30, 2013

TAHADHARI YA UGONJWA WA NIMONIA INAYOTOKANA NA CORONA VIRUS.


Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo tarehe 22 Mei 2013, kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa Nimonia unaosababishwa na kirusi cha “Novel Coronavirus”.Taarifa hiyo inaeleza kuwa,tangu ugonjwa huo utokee mwishoni wa mwaka 2012 hadi tarehe 23 Mei 2013  idadi ya wagonjwa wapatao 44 na vifo 22 viliripotiwa

Shirika la Afya Duniani limethibitisha ugonjwa huu kuwepo katika nchi za Mashariki ya Kati  yaani Jordan, Qatar, Saudi Arabi na Falme za Kiarabu (UAE). Katika bara la Ulaya, ugonjwa huu umethibitishwa kutokea nchi za Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza. Katika bara la Afrika, ugonjwa huu umetokea Tunisia.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale wanaosafiri kuelekea maeneo tajwa yenye uthibitisho wa ugonjwa huu.

Ugonjwa huu unaenezwa na kirusi kiitwacho “novel coronavirus (nCoV).”. Dalili kuu za ugonjwa huu ni kushindwa kupumua kwa ghafla, homa kali, kukohoa, na kubanwa na mbavu na hatimaye kupata Nimonia. Dalili nyingine ambazo zinaweza kutokea ni pamoja na kupata maumivu makali ya tumbo pamoja na  kuharisha.

Vile vile ugonjwa huu unaweza kupelekea figo kushindwa kufanya kazi na hata kusababisha  kifo. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu ni kati ya siku 2 hadi 10 baada ya kupata maambukiziUgonjwa huu hauna tiba wala chanjo.

Ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Njia za maambukizo bado hazijajulikana ingawa uwezekano mkubwa wa maambukizo ni kwa kwa njia ya hewa (kukohoa/kupiga chafya) au kwa kugusa majimaji/makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

·        Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania bara. Aidha, taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),  “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli ikiwa ni pamoja na vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.    

·        Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha watalaamu hawa pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga na maambukizi ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.

·        Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili kwa wasafiri watakaokwenda au kurudi katika maeneo tajwa yaliyothibitishwa kuwa na ugonjwa huu. Vipeperushi vya ugonjwa huu vimetumwa katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.

·        Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa  namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana


·        Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini. Wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi juu ya umuhimu wa KUNAWA MIKONO VIZURI KWA SABUNI NA MAJI MARA KWA MARA na pia KUZUIA MDOMO NA PUA KWA KITAMBAA AU KARATASI LAINI  WAKATI WA KUKOHOA AU KUPIGA CHAFYA.

Pia wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.

No comments:

Post a Comment