Maalim Seif Atembelea Wafanyabiashara wa Jua Kali Saateni Zanzibar.
Mfanyabiashara wa soko la Saateni Khamis Ali
Mohd akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad kuhusiana na hali ya kudorora kwa biashara katika soko hilo, wakati
Maalim Seif alipotembelea eneo hilo jana.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad akiulizia bei ya viatu, wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo
la biashara la Saateni mjini Zanzibar.maaarufu kwa jina la jua kali.
Mfanyabiashara ya mitumba katika soko la
Saateni akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad alipotembelea eneo hilo jana.
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia biashara ya mitumba, wakati
alipofanya ziara ya kutembelea eneo la biashara la Saateni mjini Zanzibar.(Picha
na OMKR)
Makamu wa Kwanza wa
Rais Maalim Seif Atembelea Wafanyabiashara Jua Kali.
Na Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea umuhimu wa kutafutwa muwekezaji kwa ajili ya kulijenga na kuliendeleza soko la saateni, ili kuweka mazingira bora ya kibiashara katika soko hilo.
Amesema mazingira yaliyopo sasa hayaridhishi kutokana na kutokuwa na miundombinu imara, hali inayowafanya baadhi ya wafanyabiashara kufikia uamuzi wa kulihama soko hilo na kuelekea darajani, eneo ambalo haliruhusiwi kwa wafanyabiashara wadogowadogo.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya kutembelea soko la Saateni kuangalia hali ya biashara inavyokwenda hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
Amesema iwapo soko hilo litaimarishwa na kuwekewa miundombinu ya kisasa, litaweza kuwavutia wafanyabiashara wengi na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakikabiliwa na tatizo hilo.
“Dawa ya kuwadhibiti wafanyabiashara wadogo wadogo walioko darajani ni kulijenga eneo la Saateni na kuwekea miundombinu ya kisasa, wala haina haja ya kutumia nguvu, watakuja wenyewe Saateni”, alifahamisha Maalim Seif.
Aidha ameuagiza uongozi wa baraza la manispaa Zanzibar kuharakisha ujenzi wa vyoo katika eneo hilo, ili kuwaondoshea usumbufu wafanyabiashara na wananchi wanaofika katika eneo hilo.
“Naomba kwa sasa kipaumbele kiwe ni ujenzi wa vyoo kwani wananchi wanaofika katika eneo hili na wengi na bila shaka watakuwa wanasumbuka”, aliagiza.
Sambamba na hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema soko la Saateni linaweza kuimarika zaidi iwapo kituo cha daladala cha darajani kitahamishiwa katika eneo hilo.
Kwa upande wao wafanyabiashara wa Saateni wamesema hali ya biashara katika eneo hilo sio nzuri, hali inayotokana na wananchi wengi kufikia eneo la darajani na kumalizia shughuli zao za kibiashara katika soko hilo.
Wamesema ni vigumu kwa sasa wananchi kwenda katika soko la saateni kutokana na usumbufu uliopo wa daladala, na kuomba kituo cha daladala kihamishiwe eneo la Saateni ili kuwawezesha wananchi kufika moja kwa moja katika soko hilo.
“Hatuwezi kuwa na masoko mawili katika nchi hii ndogo, tunaomba kituo cha daladala kihamishiwe Saateni kama tulivyoahidiwa, na serikali kutowaonea muhali wafanyabiashara wenzetu wadogowadogo walioko darajani, wawahamishe wawalete huku tuungane la si hivyo na sisi tutarejea darajani”, alitanabahisha mfanyabiashara mmoja wa soko hilo aliyejitambulisha kwa jina la Makame Mussa.
Mfanyabiashara mwengine wa soko hilo nd. Khamis Ali Mohd amesema biashara zao zimekuwa zikiyumba kutoka na wafanyabiashara wa Darajani kuendelea kuweko huko, na eneo la Saateni kusahauliwa kabisa kibiashara.
“Mimi ni mjenzi ambaye nililazimika kujenga milango kadhaa kutokana na ahadi tuliyopewa kuwa wafanyabisahara wa darajani wote watakauja huku, hivyo nilijenga kutokana na makubalianao yetu na manispaa kuwa asilimia 50 ya milango niwakodishe wafanyabiashara wanaotoka darajani, lakini hadi leo hakuna aliyekuja”, alilalamika Khamis huku akionyesha milango yake kadhaa iliyofungwa kwa muda mrefu bila ya kufanyiwa biashara yoyote.
Amesema awali alipanga kukodisha milango hiyo kwa shilingi 70 elfu kila mmoja lakini ameshindwa kupata mteja hata wa shilingi 40 elfu, kutokana na mwenendo mbaya wa biashara unaosababishwa na kuweko kwa wafanyabiashara na kituo cha daladala katika eneo la darajani.
Ameiomba serikali kufuatilia kwa karibu uimarishwaji wa soko la Saateni, ili kulifanya kuwa soko kubwa la kisasa litakalovutia wafanyabiashara wakubwa na wadogo, na hatimaye kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Kwa upande mwengine wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuweka matuta katika eneo hilo ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mwinyihaji Makame amesema serikali inaweka utaratibu wa kuweza kuwahamisha wafanyabiashara wadogo wadogo wa darajani ili waweze kuungana na wenzao walioko Saateni.
“Ukweli soko la darajani limevamiwa, hata ukienda katika eneo linalouzwa bidhaa za vyakula, lakini imebidi tufumbie macho kidogo kwa kipindi hiki, ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaotafuta huduma mbalimbali ikizingatiwa kuwa ni mwezi mtukufu wa Ramadhani”, Alisema Dkt. Mwinyihaji Makame.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, kwa upande wake aliahidi kuimarisha mazingira ya kibiashara katika soko hilo, na kusisitiza haja ya eneo hilo kuwa ndio kituo kikuu cha daladala “bus stand”.
Hassan Hamad (OMKR).
No comments:
Post a Comment