LIGI KUU YA TANZANIA BARA KUENDESHWA NA KAMPUNI MSIMU UNAOKUJA
KWA mara ya kwanza Ligi Kuu Bara itaandika historia msimu ujao, ambapo sasa itasimamiwa na kuendeshwa na kampuni, 'Tanzania Premium League' (TPL). Hatua ya kupitisha mabadiliko hayo, ilifikiwa katika kikao cha siku mbili cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza jana, mwenyekiti wa kamati ya kuendesha mchakato wa kampuni, Wallace Karia alisema TFF imepitisha kampuni kuwa chombo huru cha kuendesha ligi hiyo itakayoanza rasmi Septemba Mosi mwaka huu.
"Tulichokuwa tunatofautiana na TFF juu ya ligi kuendeshwa na chombo huru, lakini sasa kamati ya utendaji imetoa baraka," alisema Karia."Kuna mambo madogo ya kufanyiwa mabadiliko, hata hivyo hali hiyo siyo kikwazo cha ligi kusimamiwa na chombo huru," aliongeza Kiria.
Karia alisema baadhi ya maeneo ya kufanyiwa marekebisho ni suala la muundo wa kisheria wa uendeshaji ligi na kasoro ndogo walizozibaini awali.
Kimuundo kutakuwa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa TPL, kiongozi wa juu wa klabu iliyoshinda Ligi Kuu msimu uliotangulia.
Pia kutakuwa na Makamu Wenyeviti wa Bodi watatu, ambao ni viongozi wa juu wa timu mbili zilizoshika nafasi ya pili na tatu na Makamu wa pili wa Rais wa TFF anayewakilisha klabu.
"Pia bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Ligi Kuu inahusisha wenyeviti au wakurugenzi au kiongozi wa juu wa klabu zote 14 (16) zinazocheza Ligi Kuu, ambapo kila klabu itatoa mjumbe mmoja na TFF pia itakuwa na hisa kwenye kampuni.
Wajumbe wengine wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya ligi ambao hawatapiga kura ni mjumbe mmoja kutoka Chama cha Wanasoka wa Kulipwa, Chama cha Waamuzi (FRAT), Chama cha Makocha (TAFCA0 na Wadhamini wa Ligi Kuu.
"Kutakuwa na kamati huru ya nidhamu na rufaa ambayo itateuliwa na Bodi ya wakurugenzi ya TPL kila mwaka. Maamuzi ya kamati hii yatapaswa kutekelezwa na klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu lakini yanaweza kupigwa kwenye Kamati ya Nidhamu na Rufaa ya TFF," aliongeza Kiria.
Uhusiano kati ya TPL na TFF utaruhusu Makamu wa pili wa Rais TFF kuwa makamu wenyeviti wa bodi ya wakurugenzi wa TPL.
Aidha, uchaguzi wa makamu wa rais wa TFF utafanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa TPL au UTAFOC na kiongozi huyo atapaswa kuwa ama kiongozi wa juu wa klabu ya Ligi Kuu au Ligi Daraja la Kwanza au mmoja wa wanahisa wa Klabu inayoshiriki Ligi Kuu au Daraja la Kwanza.
Kuhusiana na mapato ya milango ambayo kwa sasa TFF inachukua asilimia 10, TPL itapaswa kutoa asilimia ya hisa za TFF kutoka pato lake na klabu zitapaswa kutoa asilimia tano (5%) pato la milangoni.
Kuhusu kumiliki hisa za kampuni, klabu zote zinazocheza Ligi Kuu zitakuwa na hisa sawa kwenye kampuni, ambazo zitapatikana kutokana na klabu kuwa mwananchama, na iwapo iwapo itashuka daraja, hisa zake zitahamia kwa klabu iliyopanda daraja.
Wakati huohuo, klabu zote 14 zinazoshiriki Ligi Kuu zinatarajia kufanya kikao leo kwenye ukumbi wa JB Delmont, ambapo moja ya ajenda ni kujadili kwa kina suala la kampuni hiyo.Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine alikiri kuwapo kwa mkutano huo leo.
Msemaji wa Shirikisho la soka nchini, TFF, Boniface Wambura hakukataa wala kukubali taarifa hizo zaidi ya kusema wakati kikao cha Kamati ya Utendaji kinakutana, yeye hakuwepo ofisini.
No comments:
Post a Comment