Pages

Thursday, August 16, 2012

TAIFA STARS WATOKA SARE.

MRISHO NGASSA AIOKOA STARS NA KIPIGO BOTSWANA - YATOKA SARE YA 3-3

Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa na
Lemponye Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja. Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum Abubakar na nafasi
zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman Idd. Safari hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika 13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa mara ya kwanza. Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo/Shabani Nditi,
Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd, Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi Kazimoto.
Zebras; Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.

No comments:

Post a Comment