Gazeti la NIPASHE : Mtanzania mwingine aaga Olimpiki
Ammar Ghadiyal |
Mtanzania Ammar Ghadiyal amefuata nyayo za
bondia Seleman Kidunda kuaga mapema Michezo ya Olimpiki 2012 baada ya kutolewa
katika raundi ya kwanza ya mashindano ya kuogelea ya mita 100 'freestyle'
yaliyofanyika jijini London, Uingereza jana.
Ammar ambaye, hata hivyo, ushiriki wake ulikuwa
ni wa kujifurahisha kwavile hakufuzu na alicheza Olimpiki kupitia nafasi maalum
za upendeleo, alishindwa vibaya jana baada ya kushika nafasi ya 57 kati ya
washiriki 62 akitumia muda wa dakika 1:05.
Mashindano hayo ya awali ya wanaume yalikuwa ni
ya kusaka washindi 16-Bora ambao wamesonga mbele katika safari yao ya kuwania
medali.
Mwakilishi mwingine wa Tanzania, Magdalena
Moshi, ambaye pia hakufuzu kama Ghadiyal, anatarajia kujifurahisha leo katika
mashindano ya kuogelea ya mita 100 (wanawake).
Magdalena, kama ilivyokuwa kwa Ghadiyal,
hatapewa medali hata akishinda kwa sababu hakufuzu kwa Michezo ya Olimpiki 2012
na atashiriki kupitia nafasi maalum za upendeleo zinazotolewa na shirikisho la
mchezo huo duniani (FINA) kwa nchi ambazo zimeshindwa kabisa kuwa na muogeleaji
hata mmoja aliyefuzu.
Baada ya bondia Kidunda kudundwa kirahisi kwa
pointi 20-7 dhidi ya bondia Vasilii Belous wa Moldova katika pambano la hatua ya
awali lililofanyika juzi la kusaka washindi 16-Bora, matumaini ya Tanzania sasa
yamebaki kwa wanariadha wanne tu ambapo mwanadada Zakia Mrisho atachuana Agosti
8 katika mbio za mita 5,000.
Wanariadha wengine wa mbio za Marathon, Samson
Ramadhan, Mohamed Msenduki, na Faustine Mussa watatupa karata zao Agosti
12.
Posted by Ebou's.
No comments:
Post a Comment